Utangulizi

Parokia ya Mt. Thomas More (Mbezi Beach) iko katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam chini ya Dekania ya Mt. Thomas More katika Manispaa ya Wilaya ya Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam. Parokia hii inapakana na Parokia Jirani za Bikira Maria Mama wa Huruma, Mtakatifu Gasper De Bufalo na Mtakatifu Mikael Malaika Mkuu, Kawe.

Parokia ya Mt. Thomas More ina historia ndefu ambapo mwaka 1996 baada ya kibali cha Paroko wa Parokia ya Tegeta, waamini walianza kusali kwenye kikanisa kidogo cha Masista wa Shirika la Waabuduo Damu Azizi ya Yesu, Mbezi Beach, kilichokuwepo pale lilipo kwa sasa Kanisa la Bikira Maria Mama wa Huruma, Mbezi Beach. Baada ya Kanisa la Bikira Maria Mama wa Huruma kutangazwa kuwa Parokia mpya, bado hiyo Parokia ilionekana kuwa mbali na makazi ya waamini wengi wa Mbezi Beach na hivyo mpango ukafanyika kufanyia ibada kwenye ukanda wa pwani karibu na Bahari na hatimaye ukapatikana ukumbi kwenye makazi ya Benki Kuu ya Tanzania yaliyopo eneo hilo ambapo ibada za Jumapili ziliadhimishwa hapo.

Paroko's statement to be entered here

Father Adrian Mubezi

Mwaka 2005 Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristu tatu (03) zilikuwa zinasali pamoja katika ukumbi wa makazi ya majengo ya BOT Mbezi Beach nazo ni;

  • Mt. Thomas More
  • Mt. John Fisher
  • Familia Takatifu

Uanzishwaji wa kigango cha Mt. More

Jumuiya hizo tatu zilizotajwa hapo juu zilishirikiana na kuratibu uanzishwaji wa Kigango kwa kushirikiana na Uongozi wa Parokia ya Bikira Maria Mama wa Huruma Mbezi Beach, Dar-es-salaam.

Kigango kuitwa jina la Mt. Thomas More lilihasisiwa na moja ya Jumuiya tatu anzilishi zilizotajwa hapo juu. Baadhi ya wanajumuiya katika jumuiya hiyo walikuwa wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Mt. Thomas More ambayo baada ya kuchukuliwa na serikali ikaitwa Shule ya Sekondari ya Ihungo iliyoko Mkoa wa Kagera. Wanajumuiya wa Jumuiya zote tatu zilizotajwa hapo juu kwa pamoja walikubaliana Kigango kiitwe Mt. Thomas More na kuwakilisha mapendekezo yao kwa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Mwezi Agosti 2005, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliridhia mapendekezo yao na kuundwa kwa Kigango kipya kilichojulikana kama Kigango cha Mt. Thomas More na hatimaye hata Parokia kutumia jina la Mtakatifu huyo. Historia ya maisha na kifo chake Mt. Thomas More inapatikana katika vitabu mbalimbali, majarida mbalimbali na mitandao ya Kanisa Katoliki. Kumbukumbu yake ni tarehe 22 Juni kila mwaka.

Baada ya kuundwa kwa Kigango cha Mt. Thomas More, Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Mama wa Huruma Padri Romuald Mukandara alisitisha kutumia Ukumbi wa BOT kwa huduma za Kiroho na kushauri kutafuta eneo litakalojengwa Kanisa kwa ajili ya huduma hiyo.

Waamini wa Jumuiya hizo walianza mkakati wa kutafuta Kiwanja cha kujenga Kanisa na kufanikiwa kupata Viwanja namba 139,140 na 141 Kitalu namba. 34 vilivyoko Mbezi Beach A, Dar-es-Salaam. Ujenzi wa Kanisa dogo ulianza tarehe 19/09/2005 kwa michango ya Waamini na kumalizika tarehe 24/09/2005 kazi iliyofanyika ndani ya muda wa wiki moja na Waamini walihama kutoka Ukumbi wa BOT na kuanza kusali katika Kanisa hilo dogo tarehe 25/09/2005.

Misa ya uzinduzi wa kigango

Kigango cha Mt. Thomas More kikiwa chini ya Parokia ya Bikira Maria Mama wa Huruma kilizinduliwa rasmi tarehe 18/10/2005 katika Misa ya uzinduzi iliyoongozwa na Padri Stephano Kaombe. Wakati huo Kigango kilikuwa na jumla ya Waamini 785.

Wakati wa uzinduzi kulifanyika:

  • Harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa jipya
  • Kuunda uongozi wa Kigango kwa kuchagua Kamati Tendaji
  • Kuunda Kamati ya maendeleo ya Kigango ambayo iliundwa kutokana na viongozi wa Kigango na Kamati Tendaji za Jumuiya.
  • Kushughulikia ujenzi wa kanisa la muda kwa kufanya uboreshaji na upatikanaji wa vifaa kwa ajili ya Misa na vitu muhimu kama viti vya kutumia Kanisani.
  • Ujenzi wa choo cha muda kwa matumizi ya Waamini wakati wa Misa, na kuvunja jengo bovu lilokuwa karibu na Kanisa la muda na ambalo lilikuwa ni hatari kwa Waamini hasa watoto.

Uchaguzi wa viongozi wa kwanza

Uchaguzi wa viongozi wa Kigango ulifanyika tarehe 20/11/2005 chini ya usimamizi wa Bwana Sangu kutoka Jimboni na viongozi wafuatao walichaguliwa:

  • Marehemu Frank Makwai - Mwenyekiti wa Kigango
  • Bw. Moses Nombo - Makamu Mwenyekiti wa Kigango
  • Bw. Joseph Selesi - Katibu wa Kigango
  • Bw. Edward Sungula –Katibu Msaidizi wa Kigango
  • Bw. Kened Nyoni - Mweka Hazina wa Kigango

Jiwe la msingi

Tarehe 07/01/2006, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alikuwa mgeni rasmi, alibariki na kuweka Jiwe la Msingi katika kiwanja ambacho Kanisa la kudumu litajengwa. Tukio hilo lilishuhudiwa pia na Hayati Mh. Edward Lowasa (aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania wakati huo) kama mgeni wa rasmi.

Kigango cha Mt. Thomas More chahamishwa kutoka parokia ya bikira maria mama wa huruma

Kigango cha Mt. Thomas More kilihamishwa kutoka Parokia ya Bikira Maria Mama wa Huruma na kuwa chini ya usimamizi wa Parokia ya Mt. Gaspari del Buffalo kuanzia mwaka 2010 mpaka mwaka 2014.

Ukuaji wa kigango

Baada ya muda Jumuiya ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ilianzizishwa. Jumuiya hii pamoja na Jumuiya za Thomas More na Familia Takatifu zikagawanywa na kuzaa Jumuiya za Damu Takatifu ya Yesu, Theresia wa Mtoto Yesu na Kristu Mfalme hivyo kufanya Kigango kuwa na jumla ya Jumuiya Saba (07) kama ifuatavyo:

  • Mt. Thomas More
  • Mt. John Fischer
  • Familia Takatifu
  • Moyo Mtakatifu wa Yesu
  • Theresia wa Mtoto Yesu
  • Damu Takatifu ya Yesu
  • Kristu Mfalme

Kuteuliwa kigango cha Mt. Thomas More kuwa Parokia

Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo alikiteua Kigango cha Mt. Thomas More kuwa Parokia Teule tarehe 07 Julai 2014 na kuwa Parokia kamili tarehe 07 Julai 2015 na Paroko wa kwanza alikuwa Padri Gilbart Makuru tangu ilipokuwa Parokia Teule 2014 mpaka Julai 2015.

Maporoko wengine walioteuliwa kuongoza Parokia ya Mt. Thomas More ni kama ifuatavyo:

Jina Muda
Paroko Nicolaus Masamba Julai 2017 – Julai 2018
Paroko Audax Kaasa Julai 2018 – Julai 2022
Paroko Ladislaus Kapinda Julai 2022 – Septemba 2024
Paroko Sylivanus Bwito Septemba 2024 – Machi 2025
Paroko Aidan Mubezi Machi 2025 – Hadi sasa

Ujenzi wa kanisa jipya

Kama ilivyoelezwa hapo juu Kanisa lililojegwa hapo awali lilikuwa ni la muda. Ujenzi wa Kanisa jipya ulianza rasmi mwaka 2011. Waumini walihamasishana kuchangia ujenzi wa Kanisa jipya na muitikio ulikuwa mkubwa. Ingawa kulikuwa na changamoto nyingi zilizojitokeza hasa ukizingatia kuwa eneo lenyewe lilikuwa na bonde na udongo wa mfinyanzi, ikapelekea ramani yake ifuate umbile bonde hilo ili kuhakikisha kuwa kiwanja hicho kinatumika ipasavyo.

Ramani ya jengo hilo imegawanyika katika sehemu kuu tatu (3), sehemu ya kwanza ni chini kabisa ambapo tunasali sasa na kimpangilio pale ni ukumbi. Sehemu ya pili juu katikati ni ukumbi, ofisi ya Paroko, Paroko Msaidizi na vyama vya Kitume. Sehemu ya tatu (3) ndilo kanisa lenyewe